SHULE YA MSINGI YA KOPOCH POKOT MAGHARIBI YANUFAIKA NA MSAADA WA CHAKULA KUTOKA AFISI YA MKEWE RAIS.

Mkewe gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin, Scovia Kachapin amepongeza afisi ya mkewe rais Rachael Ruto kwa msaada wa chakula ambao inaendelea kutoa kwa shule mbali mbali nchini kupitia mpango wa mama doing good.

Akizungumza wakati wa kuzindua chakula hicho kwenye shule ya msingi ya Kopoch eneo bunge la Kapenguria, Scovia alisema kwamba hatua hii ni muhimu zaidi katika kuhakikisha wanafunazi wanasalia shuleni hasa wakati huu ambapo jamii nyingi zinakumbwa na changamoto ya kupata chakula.

Aidha alitoa wito kwa wahisani zaidi kujitokeza na kufuata mkondo huo ili kuhakikisha kwamba hamna mwanafunzi ambaye anasitisha masomo kwa sababu ya njaa.

Namshukuru sana mama wa taifa kwa kutupa huu msaada wa chakula kupitia mpango wa mama doing good. Hatua hii itasaidia pakubwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanahudhuria masomo bila ya kuwa na wasiwasi ya chakula. Tunaomba wahisani zaidi kujitokeza kufuata mkondo huu.” Alisema Bi. Kachapin.

Kwa upande wake afisa katika afisi ya mkewe rais Nevile James alisema lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasalia shuleni, na pia kuvutia idadi kubwa ya watoto shuleni ili kuimarisha viwango vya elimu miongoni mwa shule kaunti hiyo.

“Lengo kuu la mpango huu ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wengi wanahudhuria masomo pamoja na kuwavutia wanafunzi zaidi shuleni ili kuimarisha viwango vya elimu kaunti hii.” Alisema James.