SHUGHULI ZA MASOMO KUREJELEWA JANUARI KWENYE SHULE ZILIZOATHIRIKA NA UTOVU WA USALAMA POKOT MAFGHARIBI.
Waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki amewahakikishia wakazi wa maeneo ambako shughuli za masomo zilisitishwa kufuatia utovu wa uslama katika kaunti ya Pokot magharibi kwamba shughuli za masomo zitarejelewa mwezi januari mwaka ujao.
Akizungumza eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet, Kindiki alisema kwamba kwa sasa wanaendelea kutathmini maswala yanayohitajika kabla ya shughuli ya kukarabati shule zilizoharibiwa na wahalifu kuanza juma lijalo.
“Kuna shule tano ambazo ziliathirika na utovu wa usalama eneo hili na sasa imekuwa zaidi ya mwaka mmoja hakujakuwa na masomo katika shule hizo. Tumekuja hapa kuwahakikishia wakazi kwamba lazima shule zote zifunguliwe, na hivyo kwa sasa tunatathmini mambo yanayohitajika ili kuanzia wikli ijayo tuanze kurekebisha shule zilizoharibiwa.” Alisema Kindiki.
Aidha Kindiki alisema tayari wameidhinisha maafisa 205 wa akiba NPR ambao watahudumu chini ya vikosi vya polisi na jeshi katika kuhakikisha usalama maeneo hayo, shule zilizoathirika kutokana na utovu wa usalama zikipewa kipau mbele katika kulindwa na maafisa hao.
“Tumeidhinisha maafisa 205 wa NPR ambao watafanya kazi chini ya maafisa wa polisi na jeshi ambalo linaendeleza oparesheni hapa. Kwa hivyo shule hizi ambazo ziliathirika zitapewa kipau mbele katika kupata ulinzi kutoka kwa hawa maafisa wa NPR.” Alisema.
Wakati uo huo waziri Kindiki alisema wataandaa kikao na tume ya huduma kwa walimu TSC ili kuhakikisha shule hizo zinapata walimu wapya, baada ya wale waliokuwa wakihudumu katika shule hizo kuhama kufuatia utovu wa usalama, huku wizara ya usalama ikihakikisha kuna chakula kwa ajili ya wanafunzi hao.
“Tutaketi na tume ya huduma kwa walimu TSC ili tupatiwe walimu wapya watakaowahudumia watoto hawa kwa sababu walimu waliokuwa wakihudumu katika shule hizo walienda kwingine kwa sababu za kiusalama. Vilevile wizara ya usalama itatoa chakula kwa wanafunzi watakaosomea katika shule hizi.” Alisema.