SHUGHULI ZA MASOMO KUATHIRIKA TENA KATIKA SHULE ZITAKAZOTUMIKA KAMA VITUO VYA KUPIGIA KURA.
Shule za kutwa kwenye maeneo ambako kutafanyika uchaguzi jumatatu wiki ijayo zitafungwa kwa siku moja ili kupisha shughuli hiyo muhimu.
Akitangaza hayo waziri wa elimu prof. George Magoha alisema wanafunzi kwenye kaunti za Kakamega na Mombasa, vile vile kwenye maeneo bunge ya Pokot kusini na Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi watasalia nyumbani siku moja.
Katika taarifa Magoha alisema wanafunzi wa kutwa kwenye shule za mabweni watasalia nyumbani huku wale wanaokaa shuleni wakitakiwa kusalia kwenye mabweni yao siku hiyo.
“Hatuhitaji kupoteza tena wakati wa watoto wetu shuleni na hivyo tumeelewana kama serikali kwamba shule za mabweni hazitafungwa. Wanafunzi watasalia kwenye mabweni yao katika shule ambazo zitatumika kama vituo vya kupigia kura.” Alisema.
Magoha aliongeza kuwa,”Katika shule za kutwa natumai kwamba siku moja haitoathiri lolote. Kwa shule ambazo zitatumika kupiga kura wanafunzi katika shule hizo watasalia nyumbani jumatatu na kisha kurejea shuleni jumanne.”
Aidha Magoha amesema iwapo shughuli ya kuhesabu kura italazimika kuendelea kwa siku nyingine, shughuli hiyo itafanyika kwenye vyuo vilivyoko karibu ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kuendelea na masomo yao.
“Katika hali ambapo shughuli ya kuhesabu kura itaendelea hadi siku itakayofuata, maafisa wa kusimamia uchaguzi watalazimika kukamilishia shughuli hiyo katika vyuo ambavyo vitakuwa karibu ili kuruhusu watoto wetu kuendelea na shughuli za masomo.” Alisema.
Maeneo mengine ambako uchaguzi huo unatarajiwa kuandaliwa ni maeneo bunge ya Rongai katika kaunti ya Nakuru, Kitui Rural na vile vile katika wadi za kwa njenga jijini Nairobi na Nyaki magharibi kwenye kaunti ya Meru.