SHUGHULI ZA MASHIRIKA YASIYO YA SERIKALI ZAANZA KUZAA MATUNDA POKOT MAGHARIBI.
Miradi ya kilimo ambayo ilianzishwa katika kaunti ya Pokot magharibi na mashirika yasiyo ya serikali kuanzia mwaka 2020 ikiwemo ile ya unyunyiziaji maji mashamba na kuhusisha makundi mbali mbali ya wakulima imeafikia ufanisi mkubwa katika maeneo ambako miradi hiyo inaendeshwa.
Akizungumza katika kikao cha mashirika mbali mbali kusherehekea ufanisi ambao umeafikiwa na makundi hayo ya wakulima, afisa katika shirika la SEFA Beatrice Hadeny alisema kwamba wengi wa wakulima wanaohusika katika miradi hiyo sasa wako katika nafasi bora ya kujitosheleza kifedha pamoja na chakula.
“Tumekuwa na wakulima tangu mwaka 2020 na tumefanya kazi nzuri. Wakulima sasa wanaweza kupanda vyakula mbali mbali. Tuna mradi wa unyinyiziaji maji mashamba ambapo wakulima wanapanda mimea na kutumia vyakula hivyo na pia kuuza kwa ajili ya mahitaji ya kifedha.” Alisema Hadeny.
Hadeny aidha alisema kwamba wanalenga kubuni kamati itakayohusisha wawakilishi kutoka serikali ya kaunti na mashirika yasiyo ya serikali ambayo itahakikisha shughuli za makundi hayo zinaendeshwa vyema.
“Tuna mipango ya kubuni kamati itakayohusisha wawakilishi kutoka serikali ya kaunti pamoja na mashirika yasiyo ya serikali ambayo itafuatilia shughuli za makundi haya ya wakulima ili kuhakikisha kwamba yanaendeleza shughuli zao bila tatizo.” Alisema.
Kwa upande wake naibu kamishina eneo la pokot ya Kati Jamal Ibrahim alisifia miradi hiyo akisema kwamba imechangia pakubwa hali ya usalama eneo hilo kwa kuwahusisha vijana ambao mara nyingi walikuwa wakijihusisha na visa vya uhalifu.
“Tumekuwa na tatizo la usalama eneo hili kwa muda mrefu, ila mradi huu umesaidia pakubwa katika kupunguza visa hivi kwa sababu vijana wengi ambao walikuwa wakiendeleza visa vya wizi wa mifugo sasa wamejitenga na uhalifu na kujihusisha na shughuli za kilimo.” Alisema Jamal.