SHUGHULI YA KUWAPA WAKULIMA PEMBEJEO KUFANYIKA HAPO KESHO


Wito umetolewa kwa wakazi katika kaunti hii ya Pokot Magharibi kuhakikisha wanajisajili kabla ya kupokea mbegu katika zoezi ambalo linatarajiwa kuzinduliwa kesho na gavana wa kaunti hii Prof. John Lonyangapuo.
Akizungumza afisini mwake mjini Kapenguria kaunti ya Pokot Magharibi, waziri wa kilimo na mifugo Geofrey Lipale amesema mbegu hizo zitatolewa tu kwa wakulima ambao majina yao yamesajiliwa, ili kuzuia suitofahamu ambayo huenda ikashuhudiwa.
Hata hivyo Lipale amesema huenda mbegu hiyo isitosheleze mahitaji ya wakulima huku akiwahimiza wakazi katika kaunti hii kuandaa mashamba yao tayari kwa shughuli ya upanzi wakati huu ambapo msimu wa mvua unatarajiwa kuanza.
Lipale ameomba radhi kwa kufeli kuzinduliwa shughuli hiyo iliyokuwa imeratibiwa kutekelezwa leo katika uwanja wa michezo wa Makutano kwa kile ametaja kuwa sababu zisizoweza kuepukika.