SHIRIKA LA SPECIAL OLYMPICS LAENDELEZA USAJILI WA WATOTO WENYE ULEMAVU ILI WANUFAIKE KWA ELIMU POKOT MAGHARIBI.

Wazazi eneo bunge la kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuwatoa wanao ambao wanaishi na ulemavu katika zoezi la ukaguzi wa watoto hao linaloendeshwa na shirika la special Olympics kwa nia ya kuwarejesha shuleni.

Akizungumza alhamisi wakati wa kuendeshwa zoezi hilo katika wadi ya Swam, afisa katika shirika hilo Brian Rotich alisema kwamba wanalenga watoto alfu 5 wanaoishi na ulemavu na ambao wako nyumbani ili kuwapeleka shule kwa lengo la kuhakikisha wananufaika kimasomo kama watoto wengine.

“Katika mpango huu tunalenga watoto alfu tano ambao hawaendi shuleni. Kama shirika, tunalenga kuwapeleka watoto hawa shuleni ili wao pia wanufaike na elimu kama watoto wengine katika jamii.” Alisema Rotich.

Aidha Rotich alisema kwamba baada ya kuwapeleka shule watoto hao, shirika hilo litawasaidia pia wazazi wao ikizingatiwa kwamba wanapitia hali ngumu kuwalea kutokana na unyanyapaa kutoka kwa jamii.

“Baada ya kuwasajili watoto hawa katika shule za watoto wenye mahitaji maalum, tutawasaidia pia wazazi wao ili angalau pia wakaweze kunufaika kwa sababu tunafahamu kwamba wengi wao wanakabiliwa na changamoto tele katika kuwalea watoto hawa ikiwemo kupitia unyanyapaa.” Alisema.

Kwa upande wake afisa wa maswala ya jamii katika wadi hiyo ya Swam Pari Emmanuel alipongeza shirika hilo kwa kuhakikisha kwamba watoto hao pia wananufaika kielimu, akisema hatua hiyo itawafanya kujihisi kuwa watu muhimu katika jamii.

“Mara nyingi jamii huona watoto hawa kuwa mzigo na wasio na umuhimu wowote katika jamii. Hatua kama hii ambayo imechukuliwa na shirika hili ni ya muhimu sana kwa sababu itawafanya hata wao pia kujihisi kuwa watu wenye umuhimu kwa jamii.” Alisema Pari.