SHIRIKA LA SICOM LAENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILI ATHARI ZA UKAME POKOT MAGHARIBI.

Shirika lisillo la serikali la SICOM linalenga kuzindua mpango wa kuwawezesha wakazi wa maeneo mbali mbali ya kaunti hii ya Pokot magharibi hasa kina mama ili kuweza kujikimu hasa kipindi hiki ambapo kunashuhudiwa makali ya njaa kutokana na ukame ambao umekithiri.

Afisa katika shirika hilo Winnie Cheptoo alisema kwamba lengo kuu la mradi huo ni kuwawezesha kuwa na ujuzi wa kutekeleza miradi mbali mbali ambayo itawasaidia kujikimu kimaisha wakati huu wa ukame.

Alisema kwamba shirika hilo litahusika pakubwa na utoaji mafunzo kwa makundi mbali mbali hasa ya kina mama kuhusu jinsi ya kutumia raslimali chache walizo nazo kujinufaisha wenyewe na hata jamii kwa jumla.

“Katika mradi huu tunajaribu kusaidia jamii kufanya mambo ambayo yatawasaidia kujisaidia kutokana na hali ya kiangazi. Katika mipangilio yetu tutakuwa na makundi ambayo tutakuwa tunafanyia mafunzo kuhusu maswala ya ukuzaji wa nyuki na asali, pamoja na upanzi wa mboga kwa akina mama kwa kutumia vyema maji kidogo ambayo yanapatikana.” Alisema Cheptoo.

Cheptoo alisema kwamba kina mama katika jamii ya pokot hawana usemi kuhusiana na mali ya familia kufuatia mila na tamaduni za jamii na hivyo kuwa vigumu kwao kufanya uamuzi kuhusiana na mali hiyo na hivyo mradi huo utawasaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazowakumba.

“Tunafahamu kwamba katika tamaduni zetu za Kipokot kina mama hawajakuwa na uhuru wa kumiliki mali kama vile mbuzi na ng’ombe. Hiyo inamilikiwa na waume zao ila kuku hao wanasema ni wa akina mama. Hivyo tunataka kuhakikisha kwamba kina mama wanatumia kuku kujimudu hasa wakati huu wa kiangazi.” Alisema.