SHIRIKA LA NRT, POKOT MAGHARIBI LAHIMIZA HAJA YA JAMII KUELIMISHWA KUHUSU ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI.

Mkurugenzi wa shirika la NRT kanda ya kaskazini mwa bonde la ufa Rebecca Kochulem ameelezea haja ya jamii kuhamasishwa kuhusiana athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza jumatatu baada ya kikao na wadau katika mkahawa mmoja mjini makutano kaunti ya Pokot magharibi, Kochulem alisema kwamba huenda jamii ikaathirika pakubwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi iwapo hawataweza kuelimishwa kuhusiana na swala hilo.

“Kwa sasa tunashuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi na ni muhimu kuwaelimisha jamii katika kaunti hii kuhusu hali hii ili wasiweze kuathirika zaidi katika shughuli zao za kila siku. Itakuwa vyema iwapo watakuwa na ufahamu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema Kochulem.

Kochulem alisema kwamba shirika hilo kwa ushirikiano na mashirika mengine linaendeleza miradi mbali mbali katika kaunti hiyo ambayo itawasaidia wakazi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kustahimili athari zinazotokana na mabadiliko hayo.

“Sisi kama NRT tunashirikiana na mashirika mengine katika kuendeleza miradi mbali mbali kaunti hii ambayo inapania kuwasaidia wananchi kustahimili athari za mabadiliko ya tabia nchi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wanachi wanakuwa wastahimilivu, ndio maana miradi yetu tunaiita ustahimilivu.” Alisema.

Baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wa Masol community conservancy Steven Ang’ari walielezea kunufaika pakubwa kupitia miradi ambayo inaendelezwa na shirika hilo ikiwemo miradi ya unyunyiziaji maji mashamba, kilimo cha asali miongoni mwa miradi mingine.

“Shirika hili limetufaa sana sisi kama wakulima eneo hili. Kupitia miradi ambayo inaendelezwa na NRT, wakulima sasa wana chakula cha kutosha na hata kuweza kujiendeleza kimaisha kupitia kuuza kile wambacho wanapata kupiti shughuli za kilimo.” Alisema Ang’ari.