Shirika la msalaba mwekundu lazindua kituo cha maswala ya dharura EOC Pokot magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza ushirikiano wa shirika la msalaba mwekundi na serikali yake katika kushughulikia hali tofauti ambazo zimekuwa zikitokea kaunti hiyo kufuatia majanga mbali mbali ambayo yameripotiwa.
Akizungumza katika hafla ya kuzinduliwa kituo cha maswala ya dharura katika afisi za shirika hilo mjini Kapengura, Kachapin alisema kaunti hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbali mbali zinazotokana na majanga kama vile ukame, na maporomoko ya ardhi, ila shirika hilo limekuwa msitari wa mbele kutoa misaada kwa waathiriwa.
“Kwa miaka mingi watu wetu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za ukame, maporomoko ya ardhi, mafuriko, magonjwa na hata utovu wa usalama. Lakini ni katika nyakati hizo za changamoto ambapo shirika la msalaba mwekundu limekuwa karibu nasi zaidi,” alisema Gavana Kachapin.
Aidha Kachapin alisema katika kukabiliana na hali hiyo serikali yake iliweka mikakati ya kuimarisha kitengo cha kukabiliana na majanga, ikiwemo kubuni sheria za kukipa nguvu zaidi anazosema zikitekelezwa kikamilifu zitasaidia pakubwa katika kushughulikia hali ya majanga kaunti hiyo.
“Uongozi wangu ulitambua umuhimu wa kuimarisha kitengo cha kukabili majanga, na ndipo katika mwaka 2023 tuliweka mkakati wa kubuni sheria ambazo zitasaidia pakubwa kukabili changamoto hizi iwapo zitatekelezwa kikamilifu,” alisema.
Katibu mkuu wa shirika hilo la msalaba mwekundu Ahmed Idris alisema uzinduzi wa kituo hicho ni mwanzo tu wa ushirikiano thabiti wa shirika hilo na serikali ya kaunti katika kuhakikisha huduma bora kwa wananchi, akitumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya kaunti kwa kuwekeza zaidi kwenye shirika hilo.
“Hiki kituo ambacho tumezindua hapa leo si tu jengo, au sehemu ya watu kuketi. Bali ni mahali ambapo tutatumia kuhakikisha kwamba tunaokoa maisha ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi,” alisema Idris.