Shirika la GVRC laandaa kikao na wanahabari kuangazia vita dhidi ya dhuluma za jinsia

Wanahabari kutoka kaunti ya Pokot Magharibi katika mkutano wa kuangazia jinsi ya kukabili dhuluma za kijinsia, Picha/Aswani

Na Benson Aswani,
Shirika la Gender Violence Recovery Centre GVRC limeandaa kikao na wanahabari katika kaunti ya Pokot magharibi kuangazia jinsi ya kukabili dhuluma za kijinsia.


Akizungumza katika kikao hicho ambacho kiliandaliwa katika mkahawa mmoja mjini Makutano, afisa katika shirika hilo Joel Mureithi alisema kikao hicho kilinuiwa kutoa mafunzo kwa wanahabari kuhusu visa vya dhuluma za jinsia, ili kutumia taaluma yao kuhamasisha jamii dhidi ya visa hivi.


“Tumekutana na wanahabari ili tuwe na mazungumzo na kuwafunza kuhusiana na maswala ya dhuluma za jinsia, ili waelewe kuhusu jinsi wataweza kuripoti visa hivyo katika juhudi za kuhakikisha vinakabiliwa katika jamii,” alisema Mureithi.


Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya jinsia kaunti hiyo ya Pokot magharibi Emmanuel Oigo, alisema visa vya dhuluma za jinsia ikiwemo ukeketaji na mimba za utotoni vimeendelea kuripotiwa kaunti hiyo licha ya juhudi za wadau mbali mbali kukabiliana na visa hivi.


“Visa vya dhuluma za jinsia vimeendelea kuongezeka katika kaunti hii hasa ukeketaji na mimba za utotoni. Maeneo ya pokot ya kati na pokot kaskazini ndiyo yanayoripoti visa hivi kwa wingi,” alisema Oigo.


Baadhi ya wanahabari waliohuduhuria kikao hicho wakiongozwa na Jafar Kibet walisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuhakikisha visa hivi vinakabiliwa.


“Tupo hapa ili tuwe katika nafasi bora ya kufahamu jinsi ya kuripoti visa vya dhuluma za jinsia ili tuchangie katika juhudi za serikali na washirika wake kukabili uovu huu katika jamii,” alisema Jafar.