SHIRIKA LA DNDI LAANZA KAMBI YA MATIBABU KWA MAGONJWA YALIYOSAHAULIKA POKOT MAGHARIBI.

Shirika la Drugs for Neglected diseases initiative DNDI limeandaa kambi ya matibabu katika shule ya msingi ya St. Comboni Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi kuangazia magonjwa yaliyosahaulika  kama vile kala azar na Mycetoma.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo ambayo ilianza jumatano, mkuu wa idara inayohusiana na ugonjwa wa Mycetoma katika shirika hilo Dkt. Bona Nyaoke alisema kwamba wameandaa kambi hiyo ya matibabu kuwahudumia wanaougua magonjwa hayo ikizingatiwa kwamba hayafahamiki zaidi miongoni mwa jamii.

“Tunatumia kambi hii kuangazia magonjwa haya ambayo yamesahaulika. Unakuta kwamba watu wanaougua magonjwa haya hawayaelewi, na hata madaktari hawafahamu jinsi ya kuyashughulikia, na ndiyo maana tupo hapa kuyatambua magonjwa haya na kuwashughulikia wagonjwa.” Alisema Nyaoke.

Afisa katika shirika la utafiti wa matibabu KEMRI Olga Msheti alielezea haja ya sekta mbali mbali kushirikiana kuangazia magonjwa haya ambayo yamepuuzwa licha ya kwamba yanawaathiri wakazi wengi .

Tunapojaribu kuyakabili magonjwa haya kuna umuhimu  mkubwa katika ushirikiano miongoni mwa sekta mbali mbali kwa sababu hatujakuwa tukiyaangazia. Sasa tunapasa kuyashughulikia ili kuhakikisha kwamba yanakabiliwa.” Alisema Masheti.

Kwa upande wake waziri wa afya kaunti hiyo Cleah Parklea alisema kaunti hiyo ndiyo inayoongoza katika visa vya magonjwa haya ambapo zaidi ya visa 700 huripotiwa kila mwaka, maeneo kame kama vile Seker, Lomut, Masol miongoni mwa maeneo mengine yakitajwa kuathirika.

Kaunti ya Pokot magharibi ndiyo imeathirika zaidi kwa magonjwa haya yaliyosahaulika. Kaunti hii ndiyo inayoongoza ambapo kwa mwaka huwa tunaripoti zaidi ya visa 700. Magonjwa haya hupatikana sana maeneo kame kama vile Seker, Lomut, Masol, Ombolion na kasei.” Alisema Parklea.

Wakazi wa kaunti hiyo wakiongozwa na balozi wa amani Tegla Lorupe walipongeza shirika hilo la DNDI kwa kuandaa kambi hiyo ya matibabu, wakitoa wito kwa serikali kuunga mkono shirika hilo ili kuhakikisha kwamba magonjwa haya yanakabiliwa.

“ Serikali inafaa kuunga mkono shirika hili la DNDI kushughulikia magonjwa haya kwa sababu shirika hilo pekee halitaweza. Hata hivyo tunashukuru sana shirika hili kwa ushirikiano na mengine kwa kuhakikisha kwamba watu wetu wanaougua magonjwa haya wanashughulikiwa.” Walisema. 

[wp_radio_player]