SHIRIKA LA ACF LAENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILI ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI POKOT MAGHARIBI.

Shirika la ACF limewapokeza makundi 28 ya wakulima kutoka maeneo ya Pokot ya Kaskazini, pokot kusini na pokot ya kati kaunti ya Pokot magharibi miche ya mipaipai, miembe na miparachichi katika juhudi za kupiga jeki shughuli zao za ukulima.

Akizungumza wakati wa kuyapokeza makundi hayo, waziri wa kilimo kaunti hiyo Wilfred Longronyang alisema kwamba hatua hii ni njia moja ya kukabili athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ikizingatiwa ni mimea ambayo haiathiriki pakubwa na ukame.

Longronyang aliwataka wakulima ambao wamepokea miche hiyo kuhakikisha kwamba inatunzwa vyema kwani itawafaa kwa kipindi kirefu pindi itakapoanza kuzalisha.

“Tumepokea miche ya miembe, mipaipai na miparachichi kutoka kwa shirika la ACF. Makundi 28 ya wakulima yamepokezwa miche hiyo ambayo itawafaa sana hasa wakati huu ambapo kunashuhudiwa athari za mabiliko ya anga, kwa sababu hii ni mimea ambayo haiathiriki pakubwa na ukame.” Alisema Longronyang.

Afisa katika shirika hilo Mercy Lomuk alisema kwamba lengo kuu la shirika hilo ni kuhakikisha wakazi wanakabili makali ya njaa pamoja na utapia mlo miongoni mwa watoto, wakati uo huo wakulima wakiwezeshwa kifedha kupitia kuuza matunda yatakayotokana na miche hiyo.

“Tunaamini kwamba mimea hii itakuwa na msaada mkubwa kutokana na athari za mabadiliko ya anga ambayo tunashuhudia kama taifa. Pia itafaa sana hasa kwa kuleta mapato kwa wakulima na kukabili swala la njaa na utapia mlo.” Alisemas Lomuk.

Makundi ambayo yalipokezwa miche hiyo yameelezea kunufaika pakubwa na huduma ambazo yamepokea kutoka kwa shirika hilo kando na kilimo.

“Tunashukuru sana shirika hili kwa kuwa limekuwa na manufaa makubwa kwetu sisi. Limetufunza mengi kuhusiana na maswala ya lishe bora, kilimo na sasa wametupa miche ya kupanda.” Walisema.