SHINIKIZO ZAENDELEA KUTOLEWA KUBUNI MUUNGANO MMOJA WA WANAFUNZI WA VYUO NA WALE WA VYUO VIKUU POKOT MAGHARIBI.
Ipo haja kwa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuungana na kubuni muungano mmoja.
Haya ni kwa mujibu wa aliyekuwa naibu mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi wa vyuo vikuu PUSA katika kaunti hii Daisy Chepkopus ambaye aidha ameelezea umuhimu wa kufufuliwa muungano uliokuwa ukiwaleta pamoja wanafunzi hao POCUSA.
Chepkopus alisema kwamba hatua hiyo italeta umoja miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya juu katika kaunti hii ya Pokot magharibi hali ambayo itarahisisha juhudi za kuangazia changamoto ambazo zinawakabili katika viwango tofauti.
“Kuna muungano unaoitwa PUSA ambao unajumuisha tu wanafunzi wa vyuo vikuu na kulikuwa na POCUSA ambao ulikuwa ukijumuisha wanafunzi wa vyuo vikuu na wa wale wa vyuo. Kwa hivyo ninachoomba ni kwamba warejeshe POCUSA ili wanafunzi wote wa elimu ya juu kauti hii waweze kuungana na kufanyia mambo yao pamoja.” Alisema Chepkopus
Wakati uo huo Chepkopus alitumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi wapya waliochaguliwa kusimamia muungano wa PUSA kuwawakilisha vyema wanachama wa muungano huo mbali na kuhakikisha kwamba wanashirikiana vyema na serikali ya kaunti kwa manufaa ya wanachama wake.
“Nawahimiza wote ambao wamechaguliwa kuhakikisha kwamba wanawahudumia wanafunzi wa vyuo vikuu vyema. Wasitumike na viongozi wengine na kutelekeza majukumu yao kwa wanafunzi. Pia washirikiane na serikali kwa manufaa ya wanafunzi.” Alisema.