SHINIKIZO ZA KUBUNIWA KAUNTI MPYA YA POKOT MASHARIKI ZAENDELEA KUSHIKA KASI.
Shinikizo zimeendelea kutolewa na wakazi wa jamii ya Pokot ya kubuniwa kaunti mpya ya pokot mashariki eneo la Tiati ili kuhakikisha kwamba jamii ya pokot inayoishi eneo hilo wanapata huduma za maendeleo.
Wakiongozwa na Abel Lokwete, wakazi wa eneo hilo walisema kwamba jamii ya Pokot imetengwa pakubwa katika miradi ya maendeleo hali ambayo inachangia mizozo inayoshuhudiwa na kupelekea jamii hiyo kuhusishwa na swala la utovu wa usalama.
Wakazi hao walisema suluhu ya kudumu kwa swala la utovu wa usalama ambao umekuwa kikwazo kwa maendeleo eneo hilo, ni kubuniwa kaunti mpya ambayo itapelekea jamii ya pokot kujitawala ambapo wataweza kupata raslimali zitakazopelekea kuafikiwa maswala ya maendeleo.
“Swala la maendeleo eneo hili halipo. Tunaona tu maendeleo yakifanyika maeneo mengine ila sisi hatushuhudii maendeleo haya. Kwa hivyo tumeona njia ya pekee kwetu sisi kupata maendeleo na huduma karibu nasi ni kwa kubuniwa kaunti mpya ya Pokot mashariki.” Alisema Lokwete.
Kauli yake ilisisitizwa na mshirikishi wa elimu katika shirika la Finn church aid kaunti ya Pokot magharibi Lilly Chepchumba ambaye alisema kwamba kutokana na upana wa kaunti hiyo ya Baringo, imekuwa vigumu kwa jamii ya Pokot ambayo inaishi eneo la Tiati kufikiwa kimaendeleo.
Alisema kwamba licha ya jamii ya pokot kuwa kubwa katika eneo hilo haijawakilishwa inavyostahili hali ambayo inaifanya kutengwa na uongozi wa kaunti.
“Sisi jamii ya Pokot ambao tupo Tiati tupo wengi lakini hatuna uwakilishi katika serikali, na kutokana na upana wa kaunti ya Baringo inakuwa vigumu kwetu kufikiwa na huduma za serikali eneo hili. Kwa hivyo tunaomba kwamba tupewe kaunti yetu ili nasi tupate huduma. ” Alisema Chepchumba.