SERKALI YAOMBWA KUINGILIA KATI NA KUTATUA MZOZO WA ARDHI UNAOSHUHUDIWA KANYARKWAT
Na Benson Aswani
Familia moja eneo la kanyarkwat mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na Trans nzoia wanalilia haki baada ya kufurushwa kwa boma lao na maafisa wa polisi wanaoaminika kutoka kituo cha polisi cha Kwanza kaunti ya Trans nzoia pamoja na maafisa wa NPR kutoka kolongolo kufuatia mzozo wa ardhi.
Lousikou Korii anadai kuharibiwa mali yake pamoja na kubomolewa nyumba kwa madai ya kunyakua ardhi hiyo madai anayoyakana vikali huku akisema kuwa ana stakabadhi halali zinazothibitisha kuwa alinunua ardhi hiyo kulingana na taratibu zinazostahili.
Ni kisa ambacho kimeshutumiwa na kakake Samson Korii ambaye amesema kuwa polisi hao walikosea kwa kumfurusha kakake kwani ardhi iliyo na utata ni tofauti akitoa wito kwa idara husika kuingilia kati kwani kwa sasa hamna watakakakokwenda.
Aidha amekosoa taratibu ambazo zilitumiwa na maafisa hao kumfurusha kakake katika ardhi hiyo kwani hakupewa hata notisi wala kupata maagizo kutoka mahakamani ya kumtaka kuondoka kwenye ardhi husika.