SERIKALI ZA KAUNTI ZAWATISHIA KUWAFUTA WAHUDUMU WA AFYA WANAOGOMA


Kwa sasa hatuna fedha za kushughulikia malalamishi ya wahudumu wa afya ambao wanagoma.
Ni usemi wa baraza la magavana nchini ukiongozwa na mwenyekiti wake Wycliffe Oparanya.
Oparanya amesema kuwa iwapo wahudumu hao hawatasitisha mgomo wao na kurejea kazini basi watalazimika kuwafuta kazi na kuwaajiri wahudumu wengine wa afya kwanzia wiki ijayo.
Oparanya aidha amesema kuwa ni miezi minne sasa kaunti hazijapokea fedha za maendeleo huku akisema kuwa kaunti wanahitaji kima cha shilingi bilioni 70 ili kufanikisha shughuli za kaunti.
Ikimbukwe magavana hao mapema wiki hii walisema kuwa wako tayari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wizara ya fedha baada ya wizara hiyo kuchelewa kutoa shilingi bilioni 94.7 mgao wa fedha kwenye serikali za kaunti.
Kwenye barua aliyoandikiwa waziri wa fedha Ukur Yattani, mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Wycliffe Oparanya amesema kuwa shughuli nyingi za kaunti ikiwemo mishahara ya wafanyikazi na madeni ya wanakandasi zimekwama kwa miezi minne sasa kufuatia ukosefu wa fedha hizo.