SERIKALI ZA KAUNTI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI YA KUKABILIANA NA UGONJWA WA KALA AZAR.

Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi imetakiwa kutenga bajeti ya kushughulikia ugonjwa wa kala azar ili kukabili athari za ugonjwa huo ambao mara nyingi huripotiwa katika maneo kame nchini.

Akizungumza katika hospitali ya Kacheliba wakati wa kutoa ripoti kuhusu utafiti ulioendeshwa kuhusu ugonjwa huo na Kutoa dawa kwa waathiriwa, afisa katika shirika linaloshughulikia magonjwa yaliyopuuzwa DNDI Samwel Bono alisema kuwa vita dhidi ya ugonjwa huo vinapasa kufanywa kipau mbele.

“Serikali ya kaunti inapasa kufanya kipau mbele vita dhidi ya ugonjwa huu kwa kutenga fedha katika bajeti yake ili kuushughulikia. Ujumbe huu pia nataka ufikie serikali za kaunti zingine ili tuimarishe vita dhidi ya Kala azar.” Alisema Bono.

Naibu kamishina wa eneo hilo Fredrick Ndubi alilipongeza shirika hilo kwa utafiti ambao liliendesha na ambao ulipelekea kupatikana dawa bora za kumeza na kupunguza makali ambayo waathiriwa wa ugonjwa huo walikuwa wakipitia kutokana na dawa za awali.

“Nimekuwa nikipata wagonjwa wengi wakiwa wamelala chini katika hospitali hii nikijiuliza ni kwa nini wagonjwa hawa hawawezi kuketi vyema chini. Kumbe ni kwa sababu ya makali yanayotokana na dawa ambazo zimekuwa zikitumika. Ni hatua muhimu sana ambayo DNDI imechukua ili tupunguze uchungu ambao wagonjwa wetu wanapitia.” Alisema Ndubi.

Kwa upande wake afisa wa huduma za matibabu katika hospitali ya Kacheliba Luke Kanyang’areng alisema kwamba ugonjwa huu unawapata watu wote ila kulingana na takwimu wanaoathirika zaidi ni watoto wenye umri wa kati ya miaka 5 na 12.

“Ugonjwa huu unaweza washika watu wa umri wote muradi tu ile nzi ikupate nje kwa yale masaa ambayo inatafuta damu. Ila wanaoathrika zaidi kulingana na takwimu zilizopo ni watoto wa kati ya miaka 5 na 12.” Alisema Kanyang’areng.