SERIKALI YATISHIA KUBATILISHA LESENI ZA WANAOCHIMBA MADINI POKOT MAGHARIBI KINYUME CHA SHERIA.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imetishia kubatilisha leseni za baadhi ya wawekezaji ambao wanaendeleza shughuli za kuchimba madini maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo.

Gavana Simon Kachapin alisema wapo baadhi wa wawekezaji ambao walipewa leseni za kuendeleza uchimbaji wa madini bila kufuata taratibu zinazohitajika kisheria akisema kwamba serikaki yake itaanza karibuni mchakato wa kubatilisha leseni hizo.

“Natoa tahadhari kwa wawekezaji ambao walipewa leseni bila kufuata taratibu zinazohitajika kisheria kwamba tutaanza mchakato wa kubatilisha leseni hizo.” Alisema Kachapin.

Kachapin alisema kwamba kaunti ya Pokot magharibi ina raslimali nyingi ambazo iwapo zitatumika vyema wakazi watanufaika, na kwamba kwa ushirikiano na serikali kuu na wadau wengine wataweka mikakati ya jinsi ya kuhakikisha zinatumika vyema kwa manufaa ya wakazi.

Kaunti hii ina raslimali nyingi. Madini ambayo yako kaunti hiio ni mengi sana. Na tunatarajia kwa awamu hii ya tatu ya serikali ya kaunti kwa ushirikiano na wadau wengine lazima tutumie vyema raslimali zilizo katika kaunti hii.” Alisema Kachapin.

 Wakati uo huo gavana Kachapin alisema visa vya utovu wa usalama maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo ya vitapata suluhu iwapo raslimali hizi zitatumika vyema kwani wakazi wengi watapata ajira na wengine kupata makao ya kudumu.

“Shida zote ambazo zinashuhudiwa meneo ya mipakani zitaisha iwapo tutamia vyema raslimali nyingi zilizo katika kaunti hii.” Alisema.