Serikali yatakiwa kuweka mikakati ya kukabili baa la njaa Turkwel

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi wengi wa eneo la Turkwel kaunti ya Pokot magharibi wanakabiliwa na njaa kutokana na kutokuwepo na mikakati ya kuwahusisha katika shughuli za kilimo cha mimea, na hivyo kuwafanya wengi wao kutegemea mifugo.
Naibu spika katika bunge la kaunti hiyo Victor Siywat ameelezea haja ya kuanzisha mradi wa unyunyiziaji maji mashamba ili kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kujihusisha na kilimo.
Siywat alisema kwamba maji mengi ya mto Turkwel yanapotea bure wakati ambapo yangetumika katika miradi ya kilimo ili kuwafaa wakazi wa Turkwel na kukabili baa la njaa ambalo hushuhudiwa eneo hilo mara kwa mara.
“Kila wakati kunashuhudiwa njaa eneo la Turkwel, na si kila wakati njaa husababishwa na kutokuwepo mvua. Wakati mwingine ni kukosekana mikakati ya kukabiliana na njaa. Mimi nahimiza serikali kuu kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji mashamba ili wakazi waache kutegemea mifugo na wajihusishe na kilimo cha mimea,” alisema Siywat.
Hata hivyo Siywat alipongeza hatua ya serikali ya kaunti kuwapa wakazi wa eneo hilo msaada wa chakula, akitoa wito kwa wahisani zaidi kujitokeza kuwasaidia wakazi wa eneo hilo, japo akisisitiza mikakati ya muda mrefu kukabili tatizo la njaa.
“Nataka kumshukuru gavana kwa kuwapa wakazi wa eneo hilo chakula cha msaada. Na nawahimiza wahisani kujitokeza ili kuwasaidia wakazi hao,” alisema.