SERIKALI YATAKIWA KUWATUMIA VIJANA WALIOASI WIZI WA MIFUGO KATIKA KUWAKABILI WAHALIFU BONDE LA KERIO.
Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Prof. John Lonyangapuo amependekeza kutumika vijana walioasi wizi wa mifugo kuwa maajenti wa serikali katika kuhakikisha amani inadumishwa katika kaunti za bonde la kerio.
Lonyangapuo alisema kwamba vita dhidi ya uhalifu katika kaunti hizi vitafaulu pakubwa iwapo serikali itawatumia vijana hawa kubaini wanaoendeleza uhalifu huo, na jinsi wanavyouendeleza, akisisitiza kwamba wana habari muhimu ambazo huenda zikasaidia katika kuwakabili wahalifu hao.
Aidha Lonyangapuo aliitaka serikali kuanzisha mpango wa kuwasaidia vijana ambao wanaasi wizi wa mifugo kuendeleza maisha, hatua anayosema kwamba itawavutia wengi wanaojihusisha na hulka hiyo ambayo ndiyo chanzo cha utovu wa usalama kwenye kaunti za bonde la kerio kurekebika.
“Hao vijana ambao waliasi wizi wa mifugo wanaweza kutumika vizuri sana na serikali katika kukabili uhalifu bonde la kerio. Hao ndio wanaofahamu jinsi wahalifu wanafanya shughuli zao na habari ambazo watatoa kwa serikali zinaweza kusaidia kuwakabili wahalifu hawa.” Alisema Lonyangapuo.
Wakati uo huo Lonyangapuo alipendekeza kuanzishwa mpango wa kuwafidia wakazi ambao wamepoteza mifugo yao kupitia visa vya wizi wa mifugo jinsi inavyofanya serikali ya taifa jirani la Uganda, hasa ikizingatiwa majina yao yapo katika rekodi za serikali.
“Kuna watu wengi sana wamepoteza mifugo yao na sasa wanaishi katika hali ya umasikini. Serikali ina majina ya watu hawa na ingekuwa bora iwapo ingewafidia jinsi ambavyo serikali ya Uganda inafanya kwa watu wake wanaopoteza mali yao mikononi mwa wahalifu.” Alisema.