SERIKALI YATAKIWA KUSHUGHULIKIA KWA DHARURA UTATA UNAOKUMBA ARDHI YA CHEPCHOINA.
Mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto ameitaka serikali kuchukua hatua za kushughulikia utata unaokabili ardhi yenye utata ya Chepchoina mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti ya Trans nzoia.
Moroto alisema kwamba kwa muda sasa wakazi katika ardhi hiyo wamehangaishwa ambapo baadhi wamelazimika kufurushwa kwa madai ya kuishi kwenye ardhi hiyo kinyume cha sheria, licha yao kugharamika zaidi kununua ardhi walimokuwa wakiishi.
Moroto alidai huenda kuna watu ambao wanaendeleza utapeli kwa kuchapisha hati miliki ghushi kwa nia ya kuwatapeli wananchi akiapa kuhakikisha waathiriwa wanapata haki.
“Serikali inapasa kuingilia kati kuangazia hili swala la Chepchoina kwa sababu wakazi wengi kwenye ardhi hiyo wamehangaishwa na hata wengine wamefurushwa kwa madai ya kukalia ardhi ambazo si zao.Nadhani kuna wakora ambao wanachapisha hati miliki ghushi hapo chepchoina kwa lengo la kuwalaghai wananchi.” Alisema Moroto.
Kauli yake ilikaririwa na mwakilishi wadi ya Mnagei Richard Todosia ambaye alitoa wito kwa maafisa wa idara ya ardhi kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na wenzao kutoka kaunti ya Trans nzoia kuangazia tatizo hilo kwa dharura kabla ya kufikia viwango hatari.
“Maafisa wa idara ya ardhi kaunti ya Trans nzoia wanapasa kushirikiana na wale wa kaunti hii ya Pokot magharibi kushughulikia utata huu mara moja. Huenda hali hii ikawa mbaya zaidi iwapo haitasuluhishwa haraka.” Alisema Todosia.