SERIKALI YATAKIWA KUONGEZA MGAO KWA MAENEO BUNGE ILI KUFANIKISHA MIRADI KATIKA SEKTA YA ELIMU.

Baadhi ya wabunge katika kaunti ya Pokot magharibi wameitaka serikali kuu kupitia wizara ya elimu kuongeza fedha ambazo zinatengewa maeneo bunge kufanikisha miradi kwenye shule mbali mbali.

Wakiongoizwa na mbunge wa sigor Peter Lochakapong na mwezake wa Kapenguria Samwel Morot. Viongozi hao walisema kwamba kaunti ya pokot magharibi inapasa kupewa kipau mbele wakati wa kutenga fedha za miradi ikizingatiwa ni moja ya kaunti ambazo ziliachwa nyuma kimaendeleo.

“Tumejaribu hapa kugawa raslimali ambazo zinapitia katika afisi yetu kama wabunge hasa kupitia hazina ya CDF lakini hazitoshi. Kwa hivyo tungependekeza serikali kuu hasa wizara ya elimu kuongeza fedha hasa kwa eneo hili kwa sababu tulisalia nyuma sana kwa miaka mingi kimaendeleo.” Walisema.

Wakizungumza eneo la Lomut viongozi hao aidha walitaka serikali kuhakikisha kwamba shule zilizoharibiwa na wahalifu wanaoendeleza wizi wa mifugo, zinakarabatiwa ili kuruhusu shughuli za masomo kuendelea kwenye shule hizo.

Wakati uo huo waliitaka serikali kutimiza ahadi ya ujenzi wa shule mpakani pa kaunti za bonde la kerio katika juhudi za kuhakikisha wakazi kutoka kaunti hizi wanatangamana ili kutia kikomo kwa swala la utovu wa usalama baina ya jamii za kaunti hizi.

“Shule ambazo ziliharibiwa na majangili zinapasa kujengwa ili kuwaruhusu watoto wa maeneo hayo pia kurejelea masomo. Serikali pia inapasa kutimiza ahadi yake ya kujenga shule katika mipaka yetu ili kuleta pamoja wanafunzi kutoka sehemu zote za bonde la kerio kama njia moja ya kuleta utangamano miongoni mwa jamii za eneo hili.” Walisema 

Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la Pokot magharibi Martine Sembelo aliitaka idara ya usalama kuendelea kuimarisha usalama maeneo hayo ya mipakani ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kupata elimu bila kuhangaishwa na wahalifu.

Tunaitaka idara ya usalama kuimarisha amani kila sehemu hasa maeneo ya mipakani ili kuruhusu shughuli za masomo katika shule za maeneo hayo kuendelea.” Alisema Sembelo.