SERIKALI YATAKIWA KUONGEZA IDADI YA VITUO VYA POLISI TIATI.

Pana haja ya serikali kupitia wizara ya usalama wa kitaifa kuongeza idadi ya vituo vya polisi katika eneo bunge la Tiaty ili kuimarisha usalama.

Ndio usemi wake mbunge wa mogotio Reuben Kiborek ambaye anasema kwamba eneo bunge lake lipo na idadi kubwa ya vituo vya kiusalama licha ya kuwa na idadi ndogo ya visa vya utovu wa usalama.

Kiborek anataka serikali kuungana na viongozi na wananchi ili kuleta suluhu ya kudumu kwa tatizo hili bila kurushiana lawama.

“Sisi hatuna tatizo la usalama eneo hili. Ni kwa nini kuwe na vituo nane vya polisi wakati eneo la Tiati linahitaji vituo kama 20? Si hawa polisi wapelekwe Tiati waimarishe usalama wa wakazi?” Alisema Kiborek.

Mbunge kiborek ametaja ujenzi wa shule, hospitali na miradi ya ukulima kuwa bora katika kuwakomesha wizi wa mifugo.

“Kama njia moja ya kukabili visa vya wizi wa mifugo ambavyo vimesababisha utovu wa usalama eneo la Tiati, serikali inapasa kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, barabara, makanisa, vituo vya polisi ili eneo hilo pia liendelee kama maeneo mengine.” Alisema.