SERIKALI YATAKIWA KUNUNUA MAHINDI NORTHRIFT NA KUWAPELEKEA WANAOKABILIWA NA MAKALI YA NJAA.

Kanisa la Kianglikana Diosisi ya Kitale kaunti ya Trans nzoia limetoa wito kwa serikali kuingilia kati kwa haraka na kusaidia kwa kuwapa chakula waathiriwa wa baa la njaa na kiangazi maeneo mbalimbali nchini.

Kwenye mkao na wanahabari kwa niaba ya Askofu wa Kanisa hilo Dr Emmanuel Chemengich, Kasisi Meshack Kosgei aliitaka serikali kununua mahindi kutoka kwa wakulima kanda ya North rift na magharibi mwa Kenya na kupeleka maeneo yaliyoathirika pakubwa na janga hilo.

“Tunaitaka serikali kuja kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa eneo hili la Northrift na western ambapo sasa wakulima wamevuna mazao yao na iwapelekee wenzetu ambao wanahangaika na njaa huko Turkana na maeneo mengine nchini.” Alisema Kosgei.

Kosgei aliongeza kwa kusema kwamba, “Hatuoni haja ya serikali kuanza kusema kuwa inatarajia kuagiza mahindi kutoka mataifa ya nje ili kukimu mahitaji ya wakazi maeneo hayo hali kuna mahindi ya kutosha huku.” 

Wakati uo huo Kosgei alitoa wito kwa wahisani kuungana na kanisa hilo kutoa vyakula mbalimbali vitakavyotolewa kwa  waathiriwa maeneo ya Mararal na Turkana juma hili.

“Tunaendeleza kampeni ya kukusanya chakula kwa ajili ya wenzetu wanaokabiliwa na njaa hadi ijumaa wiki hii. Tunatoa wito pia kwa wahisani mbali mbali kujitokeza kutusaidia katika shughuli hii ili tuweze kuokoa maisha” Alisema.