SERIKALI YATAKIWA KUKOMA KUWAHANGAISHA WAFANYIBIASHARA POKOT MAGHARIBI.
Chama cha wafanyibiashara chamber of commerce kaunti ya Pokot magharibi kimetoa wito kwa serikali ya kaunti kushirikiana vyema na wafanyibiashara na kutowadhulumu katika shughuli zao za kila siku.
Mwenyekiti wa chama hicho Mark Lotee alisema kwamba wafanyibiashara ndio nguzo muhimu kwa uchumi wa kaunti hiyo kutokana na ushuru ambao wanalipa, na wanafaa kushughulikiwa kwa heshima hasa na askari wa kaunti anaosema wamekuwa kero kwa wafanyibiashara.
“Serikali ya kaunti ijitolee kufanya kazi na wafanyibiashara na kukoma kuwahangaisha, kwa sababu hao ndio nguzo muhimu kwa uchumi wa kaunti hii. Askari wa kaunti wanafaa kuwashughulikia kwa heshima.” Alisema Lotee.
Aidha Lotee alitoa wito kwa serikali kuwatengea sehemu ya kufanyia shughuli zao wafanyibiashara ambao hawana sehemu maalum.
Wakati uo huo aliirai serikali kuwapunguzia kiwango cha fedha za kulipia leseni hasa ikizingatiwa wakati huu ambapo watu wengi wanapitia hali ngumu ya maisha hali ambayo imepelekea biashara kurudi chini.
“Serikali ya kaunti ije na mkakati mwafaka wa kutengea sehemu wafanyibiashara ambao hawana pahali maalumu pa kufanyia shughuli zao. Pia tunaomba kwamba leseni ya kufanyia biashara isiwe juu ikizingatiwa sasa biashara iko chini sana kufuatia hali ngumu ya maisha.” Alisema.