SERIKALI YATAKIWA KUIPA KIPAU MBELE KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI KATIKA USAJILI WA WALIMU.

Serikali imetakiwa kuwekeza zaidi katika elimu kaunti ya Pokot magharibi ili kuiwezesha kufikia viwango vya kaunti zingine nchini ikizingatiwa ilisalia nyuma zaidi kwa kipindi kirefu.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya maji na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa John Lonyangapuo viongozi wa kaunti hiyo waliitaka serikali kutoa nafasi kwa kaunti hiyo kusajili shule zaidi ili kuwapa nafasi ya masomo wanafunzi wengi.

“Huu ni wakati wetu. Tuendelee kusajili shule ikiwezekana ili watoto wengi wasome. Kwa muda tumesalia nyuma sana na ni wakati ambapo tunafaa kuwa kiwango kimoja na kaunti zingine.”Alisema Lonyangapuo.

Naye naibu spika wa kaunti hiyo Victor Siywat aliitaka serikali kuipa kipau mbele kaunti hiyo katika zoezi la usajili wa walimu linalotarajiwa akisema kwamba kaunti ya pokot magharibi ina upungufu mkubwa wa walimu ikilinganishwa na kaunti zingine.

“Najua kwamba kazi nzuri itaendelea katika zoezi la usajili wa walimu linalotarajiwa. Ila nataka tu kaunti hii iangaziwe zaidi kwa sababu tuna upungufu mkubwa sana wa walimu.” Alisema Siywat.

Mwakilishi wa akina mama Rael Aleutum alitoa wito kwa kaimu mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti hiyo Jane Nyakoe kuhakikisha kwamba asilimia kubwa ya walimu watakaosajiliwa katika zoezi hilo wanakuwa wakazi wa kaunti hiyo.

“Mkurugenzi wa tume ya TSC kaunti hii alistaafu na alifanya kazi nzuri sana. Kwa hivyo namwambia dadangu anayehudumu kikaimu katika tume hiyo kwamba wakazi wa kaunti hii wapewe kipau mbele katika usajili wa walimu unaotarajiwa.” Alisema Aleutum.

Kwa upande wake Nyakoe alisema kwamba kuna upungufu wa walimu 1,740 katika shule za msingi huku shule za upili zikihitaji walimu 886.

“Ni kweli kuna upungufu mkubwa sana wa walimu kaunti hii. Ilivyo sasa tuna upungufu wa walimu 1,740 katika shule za msingi, 1,010 katika shule za sekondari ya msingi na 886 katika shule za upili. Kwa hivyo tunapasa kupata nafasi zaidi za walimu kaunti hii.” Alisema Nyakoe.