SERIKALI YATAKIWA KUINGILIA KATI KUSAIDIA IDADI KUBWA YA WAKAZI WA WEIWEI WANAOKABILIWA NA BAA LA NJAA.

Mwakilishi wadi ya Weiwei kaunti ya Pokot magharibi David Moiben ametoa wito kwa serikali kuu kuingilia kati na kutoa chakula cha msaada kwa wakazi wa eneo hilo ambao wanakabiliwa pakubwa na makali ya njaa.

Akizungumza baada ya kuongoza shughuli ya kusambaza chakula kwa wakazi hao kilichotolewa na serikali ya kaunti, Moiben alisema serikali ya kaunti pekee haitaweza kutosheleza mahitaji ya wakazi wa eneo hilo ikizingatiwa idadi kubwa ya wakazi wanaohitaji chakula cha msaada.

“Nashukuru serikali ya kaunti kwa msaada huu wa chakula kwa wakazi wa eneo hili,. Naomba serikali kuu pia kuingilia kati na kutusaidia kwa sababu ni wakazi wengi wa eneo hili wanaohitaji msaada wa chakula na serikali ya kaunti pekee haitaweza kuwatosheleza hawa watu wote.” Alisema Moiben.

Msimamizi wa wadi ya Weiwei Christine Kalekamur alielezea haja ya serikali kuongeza kiwango cha chakula ambacho kinatolewa kwa shule za eneo hilo ili kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo kwani kwa sasa kuna changamoto ya kuendeleza shughuli za masomo kufuatia makali ya njaa.

“Viwango vya njaa eneo hili viko juu sana hadi masomo shuleni yanatatizika. Ingawa kuna chakula ambacho kimetolewa kwa shule, kiwango hicho kinahitaji kuongezwa ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanahudhuria masomo.” Alisema Kalekamur.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo shughuli za kilimo zimekwama kutokana na ukame ambao unashuhudiwa, wakisalia kutegemea uchomaji makaa ili kujikimu kimaisha, wakitoa wito kwa serikali kuanzisha mradi wa unyunyiziaji maji mashamba ili angalau wajitegemee kwa kukuza mimea.

“Sisi huku tumeshindwa kuendeleza kilimo cha mimea kutokana na ukame ambao umeshuhudiwa kwa muda mrefu. Sasa tunategemea tu uchomaji makaa kwa pato letu la kila siku. Tungeomba serikali angalau ianzishe mradi wa unyunyiziaji maji mashamba ili pia tuwe katika nafasi ya kukuza mimea.” Walisema.