SERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA USALAMA WA WALIMU MAENEO YANAYOSHUHUDIA UVAMIZI.

Viongozi mbali mbali katika kaunti ya Pokot magharibi wamelaani vikali kisa ambapo mwalimu wa shule ya upili ya Turkwel alivamiwa na majangili na kujeruhiwa vibaya mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na Turkana.

Wakiongozwa na naibu spika wa bunge la kaunti hiyo Victor Siywat, viongozi hao walidai uvamizi huo uliotokea mapema juma hili ulitekelezwa na wavamizi kutoka kaunti jirani, wakisema huenda visa Kama hivi vikawatia hofu walimu kufunza maeneo hayo iwapo hawatahakikishiwa usalama wao.

“Huyo mwalimu alipigwa akaumizwa vibaya sana na tunavyozungumza sasa yumo hospitalini akipigania maisha yake. Nataka kuiomba serikali kuu kwamba walimu wanaofunza katika maeneo ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama wahakikishiwe usalama wao. Kwa sababu visa kama hivi vitawafanya walimu wengi kuhofia kuhudumu maeneo hayo.” Alisema Siywat.

Aidha Siywat ambaye pia ni mwakilishi wadi ya Endough aliwataka maafisa wa usalama kuendesha uchunguzi wa kina na kuwakamata waliomvamia mwalimu huyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kando na kuhakikisha visa Kama hivi havishuhudiwi tena.

“Vitengo vya usalama eneo hilo vihakikishe kwamba hakutashuhudiwa tena kisa kama hiki. Wale ambao walitekeleza uvamizi dhidi ya mwalimu huyu watafutwe na washitakiwe kwa sababu hiyo ni kuhatarisha maisha ya walimu wetu.” Alisema.

Wakati uo huo Siywat alitumia fursa hiyo kushutumu kisa Cha kuuliwa mwakilishi wadi ya Kisa mashariki kaunti ya Kakamega Stephen Maloba, akitoa wito kwa serikali kuwapa waakilishi wadi walinzi wa kutosha jinsi ilivyo kwa viongozi wengine nchini.

Sisi wawakilishi wadi pia ni viongozi kama vile wabunge katika bunge la kitaifa na seneti. Hivyo tunataka kupewa pia walinzi kwa sababu kitendo cha kuuliwa mwakilishi wadi ya Kisa mashariki kinadhihirisha wazi kwamba maisha yetu yamo hatarini.” Alisema.