SERIKALI YATAKIWA KUHAKIKISHA USALAMA ENEO LA SEKER POKOT MAGHARIBI.


Chifu wa seker eneo la Sigor katika kaunti hii ya Pokot magharibi Charles Chebushen ameelezea haja ya kupelekwa vitengo vya usalama eneo hilo ili kuhakikishia wakazi wa eneo hilo usalama wao.
Akizungumza na kituo hiki Chebushen amesema kuwa eneo hilo lina idadi kubwa ya wakazi ila hamna vitengo vya usalama hali ambayo inaliweka katika hatari ya kukumbwa na utovu wa usalama iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka.
“Seker ina kata nne, moja upande wa chini na kisha upande wa juu kuna nne. Hatuna kitengo cha usalama eneo la juu na idadi ya watu ni ya juu mno na ni vigumu sana kukaa bila vyombo vya usalama. Ombi langu ni kwa serikali ihakikishe kuwa maafisa wa usalama wanahudumu pia eneo hili kuwahakikishia wakazi usalama wao.” Alisema.
Aidha Chebushen amemtaka mbunge wa eneo bunge la Sigor Peter Lochakapong kufuatilia utekelezwaji wa chapisho la gazeti rasmi la serikali kuhusu kubuniwa kata Zaidi eneo la Seker hatua ambayo itapelekea kuletwa huduma muhimu karibu na mwanachi na kubuni nafasi za ajira kwa wakazi.
“Ningependa kuomba mbunge wetu afuatilie na kuhakikisha kuwa tangazo la gazeti rasmi la serikali kuhusu kubuniwa kwa kata zaidi eneo hili linatekelezwa ili huduma za muhimu ziwe karibu na mwananchi.” Alisema.
Wakati uo huo chifu huyo amelalamikia hatua ya kuvamiwa msitu wa Seker na baadhi ya wakazi akitoa wito kwa serikali kuwafurusha wanaoishi kwenye msitu huo ili kukabili mabadiliko ya hali ya anga.
“Watu wamevamia msitu wa Seker na ikisalia hivyo italeta tatizo la uhaba wa maji. Naiomba serikali ya kaunti kuwapeleka walinzi wa msitu ili wawafurushe watu waliouvamia kwa sababu tunafahamu umuhimu wa msitu.” Alisema.