SERIKALI YATAKIWA KUFUNGA VICHINJIO VYA PUNDA.
Wakulima wanaofuga punda wametakiwa kuwatunza vyema wanyama hao ambao mara nyingi wamekuwa wakitelekezwa pakubwa.
Ni wito wake afisa katika shirika lisilo la kiserikali la Farming Systems Kenya Humphrey Wafula ambaye amesema kuwa punda ana manufaa makubwa kwa mkulima na kuwa tofauti na fedha atakazopata kutokana na kuuza mnyama huyo, mkulima anaweza kunufaika pakubwa iwapo atamweka na kumtunza vyema.
Akizungumza baada ya kukutana na wakulima wa punda chini ya mpango wa linda punda daima,Wafula ameishutumu hatua ya kufunguliwa tena vichinjio vya punda, akisema kuwa hatua hii itapelekea hasara kubwa kwa mkulima anayefuga wanyama hao kwani inapelekea ongezeko la wizi wa punda.
Ni wito ambao umesisitizwa na meneja wa Lelan dairies Daudi Sirma ambaye kando na kuelezea faida za punda katika kubeba mizigo, amesema maziwa ya mnyama huyo yanatumika katika kupunguza makali ya ugonjwa wa kifua kikuu, huku akisisitiza umuhimu wa kumtunza vyema.
Baadhi ya wakulima wa punda waliohudhuria mkutano huo wameelezea jinsi ambavyo wamenufaika na mnyama huyo wakikariri wito wa kuchukuliwa hatua wale ambao wanawadhulumu wanyama hao na kisha kuwatelekeza.