SERIKALI YATAKIWA KUANZISHA OPARESHENI YA KUKABILI WIZI WA MIFUGO BONDE LA KERIO.


Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Baringo wanaitaka serikali ya kitaifa kutangaza oparesheni ya kuwakabili majangili wanaoendeleza visa vya wizi wa mifugo na mauaji katika eneo la bonde la kerio.
Wakiongozwa na mbunge wa Baringo kaskazini Joseph Makilap wamelaani uvamizi uliotekelezwa na wezi wa mifugo katika eneo la Turkana mashariki, kaunti  ya Turkana ambapo watu 11 wakiwamo maafisa wanane wa usalama waliuwawa.
Wakiongea katika wadi ya Bartabwa, viongozi hao waliongeza kuwa kufuatia uvamizi huo, serikali sasa inastahili kuchukua hatua kali ili kukabili tatizo hilo ambalo limekuwapo kutoka jadi na kutafuta suluhu ya kudumu.
Aidha makilap alisema kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa na serikali kupitia vitengo vyake vya usalama basi huenda majangili hao wakaendeleza mashambulizi katika maeneo mengine.
“Desturi ni kwamba wakivamia huko Turkana au Samburu watakuja Baringo, kwa hivyo serikali inapasa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na visa hivi. Hawa watu wamejaribu kuichokoza serikali hii ambayo naamini ina rais na naibu rais ambao watakabiliana nao.” Alisema Makilap.
Kwa upande wake aliyekuwa mwakilishi wadi eneo hilo Reuben Chepsongol amesema kuwa pana haja ya bunduku zote haramu zinazomilikiwa na wakazi kutwaliwa huku pia akikariri kwamba ana uhakikia serikali ya sasa itatafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo la ukosefu wa usalama kwenye eneo la kerio valley.
“Bunduki zote ambazo zinamilikiwa kiharamu zinapasa kutwaliwa ili wananchi wa eneo la bonde la kerio waweze kuishi kwa njia ya amani. Na tuna matumaini makubwa na serikali iliyopo kwa sasa.” Alisema.

[wp_radio_player]