SERIKALI YATAKIWA KUANDAMA WATU WACHACHE WANAOSABABISHA UTOVU WA USALAMA KERIO VALLEY.
NA BENSON ASWANI
Aliyekuwa gavana wa kwanza kaunti ya Baringo Benjamin Cheboi amesema kwamba jamii nzima haistahili kulaumiwa kutokana na utovu wa usalama unaoshuhudiwa katika eneo la bonde la kerio.
Cheboi amesema kuwa ukosefu wa usalama katika eneo hilo umechangiwa na watu wachache ambao amesema wanastahili kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Cheboi ameongeza kuwa jamii nzima haiwezi ikahusika katika uhalifu na kwamba serikali ina wajibu wa kuwatambua wanaoendeleza wizi wa mifugo, mashambulizi ya mara kwa mara na pia mauwaji ya watu wasio na hatia.
Cheboi aidha amependekeza kubuniwa sheria ambayo itatoa adhabu kali kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuharibu au kuiba mali ya watu wengine akisema kwamba hatua hiyo itasaidia kurejesha amani na utulivu katika maeneo ya bonde la ufa.