SERIKALI YASUTWA KWA KUVUNJA SHERIA KATIKA KUKABILI UTOVU WA USALAMA BONDE LA KERIO.


Polisi kwa ushirikiano na kikosi cha maafisa wa jeshi wakiendelea na oparesheni ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria pamoja na kuhakikisha wanakabiliana na wezi wa mifugo katika bonde la kerio, viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kukosoa jinsi oparesheni hiyo inavyoendeshwa.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwakilishi wadi ya Mnagei Richard Todosia, viongozi hao walisema kwamba japo wanaunga mkono juhudi za kuhakikisha kwamba wahalifu wanakabiliwa, serikali inapasa kuzingatia sheria katika kuendeleza oparesheni hiyo.
“Tunafahamu kwamba wizi wa mifugo umepelekea hasara nyingi sana eneo hili. Na sisi kama viongozi tunaunga mkono oparesheni ya kuondoa silaha mikononi mwa raia. Lakini serikali inapasa kuhakikisha kwamba inazingatia sheria katika shughuli hiyo. Si kuvunja sheria kwa kutumia majeshi, hali kama wabunge hatujaidhinisha hilo inavyotakikana.” Alisema Moroto.
Viongozi hao waliitaka serikali kutafuta mbinu tofauti ya kukabiliana na utovu wa usalama katika kaunti athirika ikiwemo kuanzisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara, shule na hata makanisa wanayosema kwamba itasaidia kukabiliana na tatizo hilo.
“Tunapasa kuketi chini kama viongozi na kufahamu nini kiini cha uvamizi huu. Kwa mafano maeneo haya hayana barabara, hakuna shule, na hata makanisa hakuna. Sasa kama hakuna hata barabara, hayo magari ya majeshi yatapita wapi kuendesha hiyo opareheni?” Alisema.
Wakati uo huo viongozi hao waliisuta serikali kwa kile walidai kutumia nguvu katika kukabili uhalifu kwa kuwakamata viongozi wa maeneo haya wakisema badala yake viongozi hawa watumike kuhubiri amani miongoni mwa wakazi katika maeneo ambayo yameathirika na utovu wa usalama.
“Kutumia nguvu kwa Kuwakamata viongozi wa maeneo haya kwa madai ya kuchochea wananchi hakutaleta suluhu yoyote. Badala yake serikali inapasa kushirikiana na viongozi hawa ili wa weze kuhubiri amani miongoni mwa wakazi.” Walisema.