SERIKALI YASHUTUMIWA KWA KUENDELEZA UBAGUZI KATIKA VITA DHIDI YA UHALIFU BONDE LA KERIO.
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia jinsi serikali inavyoshughulikia swala la utovu wa usalama katika kaunti za bonde la kerio wakidai inaendeleza ubaguzi katika kuhakikisha hali ya usalama inarejelewa katika kaunti hizi.
Wakizungumza katika hafla moja ya mchango kwenye wadi ya Endough, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Sigor Peter Lochakapong walimsuta vikali waziri wa usalama Prof. Kithure Kindiki kwa kuipuuza jamii moja katika vita hivi.
“Watu wanalia Kindiki kwa kutekeleza majukumu yake kwa ubaguzi. Sisi tulidhani Kindiki ni mtu aliyesomea sheria. Na sasa ni kwa nini anafanya kazi kwa ubaguzi? Tunataka jamii zote ziwe sawa katika jamii ya Kenya.” Walisema.
Aidha viongozi hao waliwasuta maafisa wa KDF kufuatia kisa cha wakazi watatu wa eneo la Lochacha mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana kuuliwa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia kilipuzi kinachodaiwa kurushwa eneo hilo na maafisa hao.
Waliitaka serikali kugharamia matibabu ya waliojeruhiwa katika kisa hicho, na pia kufidia familia za waliouliwa.
“Maafisa wa serikali wamesababisha mauaji ya watu wetu. Jeshi la KDF liliwarushia watu wetu kule lochacha bomu. Na kwa sababu ni watu ambao serikali ilituma hapa kuleta usalama, sisi tunataka matibabu ya waliojeruhiwa kugharamiwa na serikali na pia kufidia familia za walioaga dunia.” Walisema.