SERIKALI YASHAURIWA KUWASHIRIKISHA WENYEJI KUWATAMBUA WAHALIFU KAPEDO


Mshirikishi wa masuala ya amani katika shirika la SIKOM Peter Sikamoi ameitaka serikali ya kitaifa kuwashirikisha washikadau wote katika kuwatambua wahalifu wanaoishi miongoni mwa wanajamii.
Akirejelea oparesheni inayoendeshwa katika Eneo bunge la Tiaty baada ya uvamizi katika eneo la Kapedo, Sikamoi amesema serikali pekee haitafanikiwa kumaliza mizozo mipakani bila kuwashirikisha wenyeji.
Ameongeza kwamba mzozo huo hauna uhusiano na wizi wa mifugo bali utata wa mipaka ndio chanzo kikuu cha mapigano hayo na kwamba serikali inafaa kuingilia kati kikamilifu.
Ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha viongozi dhidi ya kutoa matamshi ya chuki na uchochezi akisema huenda matamshi hayo yakazidisha uhasama miongoni mwa jamii hizo.