SERIKALI YAPANGA KUCHIMBA VISIMA KUKABILI ATHARI ZA UKAME POKOT MAGHARIBI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi ina mipango ya kuchimba visima katika kila wadi ambazo zimeathirika pakubwa na ukosefu wa maji kufuatia ukame ambao unashuhudiwa maeneo mbali mbali ya nchi.
Waziri wa maji, mazingira, mali asili na mabadiliko ya hali ya anga Lucky Litole alisema kwamba familia nyingi katika kaunti hiyo zinakabiliwa na changamoto ya kupata maji, na kwamba serikali ya gavana Simon Kachapin itahakikisha swala hilo linashughulikiwa jinsi alivyoahidi katika manifesto yake.
Alisema maeneo yatakayopewa kipau mbele katika shughuli hiyo ni pamoja na pokot ya kati na pokot kaskazini ambayo ndiyo yameathirika pakubwa.
“Tuna tatizo kubwa sana la maji hasa wakati huu wa ukame. Kufuatia hilo tunaendelea kuweka mikakati ya kuchimba visima katika kila wadi kwenye maeneo ambayo yameathirika zaidi hasa maeneo ya pokot ya kati na pokot kaskazini.” Alisema Litole.
Wakati uo huo Litole aliwahakikishia wananchi kwamba mradi wa maji wa Muruny-Siyoi uko katika hatua zake za mwisho na huenda ukakamilika mwezi aprili mwaka huu baada ya kupokea fedha kutoka kwa serikali kuu na ile ya kaunti zitakapotumika kukamilisha mradi husika.
“Tuko katika hatua za mwisho kwenye mradi wa muruny -Siyoi na kufikia mwezi aprili huenda ukakamilika kwa kuwa kuna fedha tunazosubiri kutoka kwa serikali kuu na ile ya kaunti zitakazotumika kukamilisha mradi huo.” Alisema.