SERIKALI YALAUMIWA KWA KUENDESHA OPARESHENI YA KIUSALAMA KWA MAPENDELEO KASKAZINI MWA BONDE LA UFA.

Mbunge wa Pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi David Pkosing ameilaumu serikali kwa kile amedai kwamba imeruhusu wakazi katika kaunti jirani kumiliki silaha kinyume cha sheria baada ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuitikia wito huo na kusalimisha silaha zao.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha habari nchini, Pkosing alisema kwamba uvamizi wa hivi punde ambao umesababisha watu wawili kuuliwa na mifugo zaidi ya alfu 2 kuibwa umetokea kutokana hali ya jamii moja kukubaliwa kusalia na bunduki huku nyingine ikipokonywa silaha hizo.

“Wakati serikali ilianzisha oparesheni ya kutwaa silaha ambazo zinamilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wakazi wa kaunti za bonde la kerio, jamii ya Pokot ilisalimisha silaha zao zote lakini wenzetu kutoka kaunti zingine walisalia na silaha zao na ndio maana wanavamia sana jamii ya pokot ambao hana jinsi ya kujilinda.” Alisema Pkosing.

Aidha Pkosing alisema huenda mfumo ambao unatumika sasa kutekeleza oparesheni katika kaunti sita za kaskazini mwa bonde la ufa  zinazokabiliwa na utovu wa usalama kufuatia wizi wa mifugo ukakosa kuzaa matunda.

“Hii mbinu ya kutuma wanajeshi kuleta usalama maeneo yanayokabiliwa na wizi wa mifugo haitafaulu. Badala yake serikali inapasa kufanya uchunguzi na kubaini hasa kiini cha mashambulizi haya ni nini kabla ya kuchukua hatua zinazofaa.” Alisema.