SERIKALI YALAUMIWA KWA KUCHOCHEA MAPIGANO YANAYOSHUHUDIWA KAPEDO


Viongozi wa kisisasa katika kaunti hii ya Pokot Magharibi wamesema kuwa serikali ndio inachochea mapigano katika eneo la Kapedo.
Wakizungumzia hatua ilizochukua wizara ya usalama kuwaandama magaidi waliowauwa maafisa wa usalama katika eneo hilo, Seneta wa kaunti hii ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Dkt Samuel Poghisio na mbunge wa Tiaty William Kamket, viongozi hao wamesema kuwa hawajahusishwa na wizara ya usalama kwenye mazungumzo ya kusaka amani licha ya mzozo huo kuathiri kaunti hii ya Pokot Magharibi, Turkana na Baringo.
Ikumbukwe kwamba hali ya usalama inazidi kudorora katika eneo la Kapedo huku miili sita ikipatikana katika eneo la Arabal kaunti ya Baringo kufuatia oparesheni inayoendelea eneo la Kapedo.
Jamii ambazo zinaishi na kupakana na Kapedo zimekuwa zikishambuliana kwa kisingizio cha wizi wa mifugo walakini uongozi wa maeneo hayo unakana sio swala la wizi wa mifugo bali mipaka ya ardhi.
Haya yanajiri huku mwenyekiti wa baraza la Maimamu na wahubiri CIPK kaskazini mwa Bonde la ufa Abubakar Bini akimtaka waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’I kuwatia nguvuni wanasiasa wanaochochea na kufadhili wizi wa mifugo katika eneo la Kapedo na kuwaajibisha kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret, Bini amesema kuwa wakenya na maafisa wa polisi hawataendelea kuuliwa kwa kupigwa risasi na mali kuharibiwa kwa faida ya watu wachache walio na malengo ya binafsi.
Bini aidha ameitaka serikali kuu kuimarisha miundo misingi ili kupiga jeki uchumi wa eneo hilo na taifa zima sawa na kuwezesha maafisa wa usalama kuimarisha usalama katika eneo la Kerio.