SERIKALI YAENDELEZA ZOEZI LA KUSAMBAZA CHAKULA SHULENI MHULA WA TATU UNAPOTARAJIWA KUAZA RASMI.

Shule mbali mbali za msingi eneo la Kipkomo katika kaunti ya Pokot magharibi zimepokea chakula kutoka kwa serikali ya kitaifa kupitia mpango wa lishe shuleni, shule zinapotarajiwa kufunguliwa juma lijalo kwa muhula wa tatu.

Akiongoza zoezi hilo naibu kamishina eneo hilo George Chege aliwahakikishia wazazi kwamba serikali itaendeleza shughuli hiyo ya kutoa lishe kwa shule ili kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanahudhuria masomo hasa wakati huu ambapo jamii nyingi zinapitia changamoto ya kupata chakula.

“Nawahakikishia wananchi kwamba serikali itaendeleza shughuli hii ya kupeleka chakula shuleni kwa sababau kinasaidia sana kuhakikisha kwamba wanafunzi wanahudhuria masomo. Kwa hivyo juma lijalo tunatarajia wanafunzi wote kuja shuleni.” Alisema Chege.

Mkurugenzi wa elimu eneo hilo la Kipkomo Evans Onyancha aliwataka walimu wakuu wa shule ambazo zimepokea chakula hicho kuhakikisha kwamba kinatumika vyema kwa malengo hitajika huku akionya kwamba hatua za sheria zitachukuliwa dhidi ya watakaohusika wizi wa chakula hicho.

“Natoa onyo kwa walimu wakuu kwamba sitaki kusikia kwamba kuna mtu yeyote ameiba chakula cha wanafunzi. Nawataka wote kuhakikisha chakula hiki kinaafikia malengo ya serikali ya kuhakikisha  wanafunzi hawapati tatizo lolote kupata chakula wakiwa shuleni.” Alisema Onyancha.

Walimu wakuu wa shule ambazo zimenufaika na chakula hicho wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha walimu wakuu wa shule za msingi KEPSHA eneo hilo Martine Musto walipongeza serikali kwa chakula hicho wakisema kitasaidia kuhakikisha wanafunzi wanasalia shuleni.

“Tunafurahi sana kama walimu kwa sababu chakula hiki kitasaidia sana watoto wetu na kuwachochea kuhudhuria masomo, ikizingatiwa kwamba jamii nyingi kwa sasa zinapitia hali ngumu kupata chakula.” Walisema.

[wp_radio_player]