SERIKALI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUWANUSURU WAKAZI KUTOKANA NA MAKALI YA UKAME POKOT MAGHARIBI.
Serikali imeanza mpango wa kununua na kuchinja ng’ombe katika kaunti hii ya Pokot magharibi kwa lengo la kuwanusuru wafugaji dhidi ya hasara ambayo husababishwa na ukame, ambapo pia inalenga kutumia nyama ya mifugo hao kama chakula cha msaada kwa wakazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo eneo la Lomut, kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Apolo Okelo amesema mpango huo unalenga jamii ambazo zimeathirika zaidi na makali ya njaa, ambapo nyama hiyo itatolewa kwa familia hizo, huku wafugaji wakipunguziwa mzigo wa kutafuta lishe kwa mifugo pamoja na kuzuia vifo kwa mifugo hao.
Alisema kuwa mpango huo utaendelezwa katika kaunti ndogo zote 4 ambako ukame umeathiri mifugo, akiongeza kuwa serikali inanunua ng’ombe mmoja kwa shilingi alfu 15,000, ambapo ng’ombe mmoja atagawiwa nyumba kumi huku nyumba alfu 13000 zikilengwa katika mpango huo.
Japo wakazi wa maeneo lengwa wamepongeza mpango huo walisema kuwa ingekuwa bora iwapo serikali ingeanzisha mradi wa unyunyiziaji maji mashamba kutokana na ukame uliokithiri, wakisema mradi huo ungewasaidia hata vijana ambao wameathirika zaidi na ukosefu wa ajira.
Apolo amesema kulingana na ukaguzi wao Zaidi ya nyumba 31,000 zimeathirika na makali ya njaa kaunti ya Pokot magharibi ambapo kila nyumba ina wanafamilia saba.
Wadi ambazo zimeathiriwa Zaidi ni pamoja na Masol, Lomut, nyanda za chini za Seker, Endough, nyanda za chini za Kasei, Kiwawa, Alale, Kapchok, Kodich, Suam, Riwo, nyanda za chini za Chepareria na Batei.