SERIKALI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA MAZINGIRA BORA KWA WATU WANAOISHI NA ULEMAVU NCHINI.
Waziri wa leba Bi. Florence Bore amesema kwamba watu wanaoishi na ulemavu nchini wameendelea kukumbwa na vizingiti ambavyo kwa miaka mingi vimewapelekea kukosa kuhusika kikamilifu katika maswala ya maendeleo na kufurahia haki zao licha ya kwamba nafasi yao ni muhimu katika idadi ya watu nchini.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya walemavu ambayo iliandaliwa jumapili katika uwanja wa makutano kaunti ya Pokot magharibi, Bi. Florence Bore alisema wizara yake itahakikisha mswada unaoangazia maswala ya watu wanaoishi na ulemavu mwaka 2023 unashughulikiwa na kuwa sheria ili kuhakikisha maslahi ya watu hao yanaangaziwa kikamilifu.
“Japo watu wanaoishi na ulemavu wanabuni sehemu muhimu sana katika idadi ya watu nchini, wangali wanakabiliwa na vizingiti ambavyo vinawazuia katika kushiriki kwenye maswala ya maendeleo na kufurahia haki zao kikamilifu.” Alisema Bi. Bore.
Gavana wa kaunti hiyo Bw. Simon Kachapin alisema kwamba japo kuna mengi ya kufanya kuhakikisha watu wanaoishi na ulemavu wanapata huduma bora zinazopasa, serikali yake imepiga hatua muhimu katika kuafikia hayo.
“Katika kaunti hii tumepiga hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba watu wanaoishi na ulemavu wanapata huduma bora. Hata hivyo tunakiri kwamba kuna kazi kubwa ambayo tunapasa kufanya kuhakikisha watu hawa wanaafikia huduma muhimu kikamilifu.” Alisema Bw. Kachapin.
Kwa upande wake afisa katika shirika la UNFPA Bi. Lilian Lang’at alielezea haja ya jamii kubadilisha dhana kuhusiana na watu wanaoishi na ulemavu, hali aliyosema kwamba inachangia pakubwa katika visa vingi vya kukiukwa haki zao hasa wale wa jinsia ya kike.
“Mara nyingi dhana ambazo zinahusishwa na watu wanaoishi na ulemavu zimewapelekea wengi wao hasa wale wa kike kupitia dhuluma mbali mbali katika jamii. Ni wakati jamii inapasa kubadili dhana hizi ili watu hawa pia wapate kuishi kufurahia haki zao.” Alisema Bi. Lang’at.
Watu wanaoishi na ulemavu wakiongozwa na Bi. Regina Chumba waliitaka serikali kuu pamoja na zile za kaunti kutenga asilimia 5 ya ajira kwa watu hao ili pia kuwafanya kuhisi kuwakilishwa.
“Tunataka serikali ya taifa na zile za kaunti kuhakikisha kwamba tunawakilisha kikamilifu kwa kututengea asilimia tano na zaidi ya nafasi za ajira.” Alisema Bi. Chumba.
Hafla hiyo pia ilishuhudia kutiwa saini mkataba wa maelewano baina ya baraza la kitaifa la watu wanaoishi na ulemavu na huduma Kenya pamoja, na usambazaji wa vifaa vya kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.