SERIKALI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUFANIKISHA MTAALA WA UMILISI CBC.
NA BENSON ASWANI
Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mtaala wa umilisi CBC unafanikishwa jinsi ilivyopangwa.
Mkurugenzi wa elimu eneo la Kipkomo kaunti hii ya Pokot magharibi Evans Onyancha amesema kuwa mipango yote ya ujenzi wa madarasa 56 zaidi katika shule 46 za upili eneo hilo ili kufanikisha mpango huo tayari imekamilika na sasa kinachosubiriwa ni mwanakandarasi kuanza shughuli hiyo.
Onyancha ameelezea matumaini ya kukamilika ujenzi wa madarasa hayo katika kipindi ambacho kimeratibiwa na serikali huku akitoa wito kwa jamii ya eneo hilo kutoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha shughuli hiyo.
Kuhusu swala la mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi wa kike, mkurugenzi huyo wa elimu amesema kuwa wameweka mikakati ya kutumia wadau mbali mbali ikiwemo viongozi wa kidini ili kutoa ushauri kwa wanafunzi hao kuhusu umuhimu wa kuepuka swala hilo na kuzingatia pakubwa elimu yao.