Serikali yaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo

Wanafunzi waelekea kupata chakula kupitia mpango wa lishe shuleni, Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi
Shule mbali mbali eneo bunge la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi zimenufaika na chakula kutoka kwa serikali katika juhudi za kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanahudhuria masomo.


Akizungumza baada ya kuongoza zoezi la kusambaza chakula hicho, mkurugenzi wa elimu eneo bunge la Kacheliba Simon Lodiang’ole amesema jumla ya shule 58 zimenufaika akitaja hali ya usafiri kuwa changamoto kubwa katika shughuli hiyo.


“Tumesambaza chakula kwa jumla ya shule 58, ingawa tumekuwa na changamoto katika kusafirisha chakula hicho kutokana na ubovu wa barabara, nyingi ya shule zimenufaika na tutafanya juhudi zote kuhakikisha shule zote zinapata,” alisema Lodiang’ole.


Alisema kwamba tangu kuanza mpango huo, idadi ya wanafunzi katika shule mbali mbali imeongezeka na kupelekea changamoto ya madarasa.


Hata hivyo alisema hali hiyo inashughulikiwa.


“Wanafunzi wameongezeka sana shuleni tangu kuanza mpango huu. Sasa tuna changamoto ya madarasa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule zetu, ila hilo tunalifanyia kazi,” alisema.


Kuhusu swala la walimu kukosa kuhudhuria vipindi vya masomo, Lodiang’ole amesema kwamba visa hivyo vimepungua pakubwa kwani kwa muda sasa hamna ripoti ambazo zinawasilishwa katika afisi yake kulalamikia hali hiyo.


“Ni muda sasa tangu tupokee ripoti kuhusu walimu ambao wanafeli kufika shuleni kuwahudumia wanafunzi. Kwa sasa naamini walimu wanafanya kazi nzuri,” aliongeza.