SERIKALI YAENDELEA KUWEKA MIKAKATI KUKABILI KERO LA UKAME

Huku hali ya ukame ukiendelea kukithiri katika baadhi ya kaunti nchini serikali ya kaunti hii kupitia idara ya kilimo inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wakazi wanapata suluhu ya kudumu kwa tatizo hilo kupitia mradi wa climate smart.

Kulingana na mkurugenzi wa idara ya kilimo kaunti hii Philip Ting’aa serikali inaendeleza uchimbaji wa mabwawa katika maeneo mbali mbali ya kaunti hii ili kufanikisha kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba katika juhudi za kuhakikisha usalama wa chakula na kukabili baa la njaa ambalo limekuwa changamoto kwa miaka mingi.

Alisema kwamba mradi unaotekelezwa katika wadi ya Sook utafanikisha kilimo katika ekari 300 za shamba na umegharimu zaidi ya shilingi milioni 40 huku ule unaotekelezwa katika wadi ya Siyoi ukigharimu kima cha shilingi milioni 26 ambayo inanuia kuwanufaisha pakubwa wakulima.

“Tuna miradi miwili ya kunyunyizia maji mashamba, wa kwanza ukiitwa Kigen Irrigation project katika wadi ya sook ambao umegharimu takriban shilingi milioni 44. Mradi mwingine ni wa Chapkoti ulio katika wadi ya Siyoi ambao umegharimu shilingi milioni 26.” Alisema Ting’aa.

Ting’aa alitoa wito kwa wakulima wa eneo hilo pamoja na kamati iliyobuniwa kufanikisha miradi hiyo kushirikiana kikamilifu na mwanakandarasi aliyejukumiwa kutekeleza miradi hiyo anayosema kwamba inatarajiwa kukamilika kufikia mwezi desemba mwaka huu.

“Nawasihi wakulima wa eneo hilo na kamati inayoshirikiana na mwanakandarasi kushirikiana ili hii miradi itekelezwe haraka maana inafaa kuwa tayari kufikia mwisho wa mwezi desemba. Nia yetu ni kuona kwamba wananchi wanasaidika ili kukabili tatizo la baa la njaa.” Alisema.

[wp_radio_player]