SERIKALI YAENDELEA KULAUMIWA KUFUATIA KUKITHIRI UTOVU WA USALAMA MPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA.
Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameendeleza shutuma dhidi ya mauaji ya mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 18 katika kijiji cha Ompolion wadi ya Kasei wakati alipokuwa akilisha mifugo.
Wakazi hao wameisuta serikali kwa kutokuwa makini na kushughulikia swala zima la utovu wa usalama hasa mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana, wakidai serikali imekuwa ikiegemea upande mmoja katika kushughulikia swala hili.
Wakati uo huo wakazi hao waliwasuta viongozi wa kisiasa kwa kile walisema kwamba ndio wanaochangia kukithiri visa vya uvamizi kwa matamshi wanayotoa wakitoa wito kwa idara za usalama kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Ni kama serikali ya kitaifa haijakuwa makini katika kukabili tatizo hili la utovu wa usalama mpakani pa pokot magharibi na Turkana. Sasa ni wananchi wenyewe wanaojitetea. Pia kuna viongozi wachache wanaochochea hali hii kwa kutoa maneno ya kiholela. Serikali inafaa kuwachukulia hatua za kisheria.” Walisema wakazi.
Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa viongozi kutoka kaunti zote za kaskazini mwa bonde la ufa kuandaa kikao cha kutafuta suluhu kwa tatizo la usalama, pamoja na serikali kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inaanzishwa maeneo haya.
“Ningeomba viongozi wa kaunti sita za kaskazini mwa bonde la ufa kuitisha mkutano baina ya jamii za kaunti hii ili wazungumze kama viongozi. Serikali pia inafaa kuhakikisha kwamba maeneo haya yanapata maendeleo kama njia moja ya kushughulikia tatizo hili.” Walisema.