SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA JUHUDI ZA KUKABILI MAKALI YA UKAME KATIKA BAADHI YA MAENEO YA POKOT MAGHARIBI.
Naibu kamishina eneo la pokot ya kati Jeremiah Tumo amesema kwamba serikali inaendelea kuweka mikakati ambayo itahakikisha kwamba ukame ambao unaendelea kushuhudiwa maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi hauwaathiri vibaya wananchi.
Akizungumza na kituo hiki Tumo alisema kwamba serikali kwa ushirikiano na mamlaka ya kukabili majanga NDMA inaongeza idadi ya watu ambao wananufaika na chakula cha msaada kutokana na athari za ukame huo.
Aidha Tumo alisema serikali inashirikiana na mashirika mbali mbali yasiyo ya serikali katika kuwashughulikia waathiriwa wa ukame ambayo kando na kusambaza chakula, yanatoa huduma mbali mbali kwa wakazi kuwaepusha na makali ya ukame.
“Kama njia moja ya kuzuia athari zaidi za ukame ambao unashuhudiwa maeneo mbali mbali ya kaunti hii, tumeongeza idadi ya watu ambao wananufaika na msaada wa chakula ambao unatolewa na serikali. Pia tunashirikiana na mashirika mbali mbali yasiyo ya serikali katika kuwafaa wakazi hawa, si kwa chakula tu bali pia kupitia miradi mbali mbali.” Alisema Tumo.
Wakati uo huo Tumo alisema tayari shule zimepokea chakula katika mpango wa lishe shuleni zinapofunguliwa juma hili kwa muhula wa tatu, ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanahudhuria masomo kikamilifu bila ya kuwa na wasiwasi wa kupata chakula.
Pia tuna mpango wa lishe shuleni ambapo kufikia sasa shule zote kaunti hii zimepokea chakula, wanafunzi wanapotarajiwa kurejelea masomo juma hili kwa muhula wa tatu. Tunafanya hivi ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanahudhuria masomo bila ya kuwa na wasi wasi ya chakula.” Alisema.