SERIKALI YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA MASHIRIKA YASIYO YA SERIKALI KUIMARISHA MAISHA YA WAKAZI POKOT MAGHARIBI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi itatenga fedha zaidi katika kipindi cha fedha kijacho ili kuimarisha shughuli za makundi mbali mbali ya wafanyibiashara wa viwango vya chini hasa maeneo ya mashinani.
Haya ni kulingana na mkurugenzi katika idara ya biashara na mashirika kaunti hiyo Jacob Kapelile ambaye amesema kuimarisha maisha ya wakazi kupitia mradi wa biashara mashinani ilikuwa moja ya manifesto ya serikali ya gavana Simon Kachapin na kwamba itahakikisha inatekeleza manifesto yake kikamilifu.
“Gavana kachapin ametenga kiasi kikubwa cha pesa kuwasaidia hasa wafanyibiashara wadogo wadogo kuimarisha biashara zao kupitia mradi wa biashara mashinani. Katika kipindi cha fedha kijacho fedha hizo zitatolewa kwa walengwa kulingana na manifesto yake.” Alisema Kapelile.
Wakati uo huo Kapelile alisema kwamba serikali ya kaunti kupitia idara ya biashara itashirikiana kikamilifu na mashirika yasiyo ya serikali katika shughuli zake ambazo yanaendeleza katika kaunti hiyo kuimarisha maisha ya wananchi.
“Kuna mashirika yasiyo ya serikali katika kaunti hii kama vile SEFA, ACF miongoni mwa mengine ambayo yanaendeleza miradi ya kuwanufaisha watu wetu. Serikali ya gavana Kachapin imeahidi kushirikiana kikamilifu na mashirika haya ili kuboresha maisha ya wananchi.” Alisema.
Aidha Kapelile aliyapongeza mashirika hayo ya kijamii kwa juhudi ambazo yameendeleza kaunti hii akisema kwamba wengi wa wakazi wa kaunti hii wamenufaika pakubwa kupitia miradi ambayo inaendelezwa na mashirika hayo.