SERIKALI YAAGIZA KUFUNGULIWA SHULE ZOTE ZILIZOFUNGWA KUFUATIA UTOVU WA USALAMA POKOT MAGHARIBI.

Waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki ameagiza kufunguliwa shule zote ambazo zilifungwa kutokana na ukosefu wa usalama katika kaunti ya Pokot magharibi ili kuwaruhusu watoto kutoka maeneo yaliyoathirika kupata nafasi ya kuhudhuria masomo.

Akizungumza eneo la Sarmach eneo bunge la sigor, Kindiki alisema serikali imetenga kima cha shilingi milioni 100 ili kufanikisha ukarabati wa shule zilizoharibiwa na wahalifu, shughuli itakayotekelezwa na maafisa wa KDF kwa ushirikiano na vijana waliofuzu kutoka shirika la huduma kwa vijana NYS.

“Tutahakikisha kwamba shule zote kaunti ya Pokot magharibi ambazo zilifungwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama zinarekebishwa na kisha kufunguliwa ili watoto wetu warudi shuleni. Serikali imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo ambao utafanywa na maafisa wa KDF kwa ushirikiano na vijana wa NYS.” Alisema Kindiki.

Aidha Kindiki alitangaza kubuniwa taarafa mpya saba katika kaunti hiyo, akisema kwamba serikali itawatuma maafisa wa utawala kwenye taarafa hizo ifikiapo ijumaa wiki ijayo kama moja ya mikakati ya kukabili utovu wa usalama katika kaunti hiyo.

“Ninaamuru kubuniwa taarafa 7 mpya katika kaunti hii, ikiwemo Chepkobes, Kodich, Seker, Masol, Kaptabuk, Miskwony na Endough ambazo zitaanza kufanya kazi wiki ijayo. Tutatuma maafisa wa utawala katika taarafa hizo ifikiapo ijumaa ili kazi ianze kutekelezwa mara moja.” Alisema.

Wakati uo huo Kindiki alitumia fursa hiyo kuwaonya  viongozi katika kaunti hiyo dhidi ya kuingiza siasa katika swala zima la usalama, akisema kwamba serikali inatekeleza jukumu lake la kuhakikisha usalama kote nchini kwa usawa.

Kwa upande wake gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alimhakikishia Kindiki kwamba kama viongozi, watashirikiana kikamilifu na serikali kuu kuhakikisha amani inarejelewa eneo hilo ili kutoa nafasi kwa miradi ya maendeleo kutekelezwa.

“Sisi kama viongozi wa kaunti hii tutashirikiana kikamilifu na serikali kuu ili kuhakikisha kwamba amani inadumishwa eneo hili ili hata sisi tupate nafasi ya kuhakikisha kwamba maendeleo yanaafikiwa kwa ajili ya wananchi wetu.” Alisema Kachapin.