SERIKALI YA UGANDA YALAUMIWA KWA KUEGEMEA JAMII YA POKOT KATIKA VITA DHIDI YA WIZI WA MIFUGO.

Aliyekuwa gavana wa wilaya ya Amudat mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda Francis Kiyonga ameilaumu serikali ya Uganda kwa kile amedai kukabili visa vya wizi wa mifugo kwa kuegemea kabila moja.

Kiyonga alisema licha ya kwamba jamii ya Pokot eneo hilo imepoteza mifugo wengi kufuatia wizi ambao unaendelea kushuhudiwa, wamekuwa wakilengwa zaidi na utawala wa taifa hilo kwa kudaiwa kuwa ndio wanaoendeleza wizi wa mifugo wa jamii ambazo wanapakana nazo.

Alisema kwamba hatua hiyo imewafanya wakazi wengi wa jamii ya pokot kuhama eneo hilo na kurejea katika kaunti ya Pokot magharibi wakihofia kuandamwa na maafisa wa usalama katika oparesheni ya kukabili wizi wa mifugo.

“Kwa miaka miwili sasa watu wetu wamepoteza mifugo wengi sana. Na serikali badala ya kufuatilia mifugo hao wanasema kwamba wapokot wameiba mifugo wa karamoja. Hali hii imewasumbua sana wa wetu na hata wengine wao wameanza kuhama kurejea Kenya.” Alisema Kiyonga.

Kiyonga aliitaka serikali ya taifa hilo kupitia idara ya usalama kuwaandama watu binafsi ambao wanaendeleza wizi wa mifugo na kutojumuisha jamii yote, akisema kwamba jamii ya pokot imekuwa msitari wa mbele kuhakikisha kwamba wezi wa mifugo wanatambuliwa.

“Watu wetu tangu kitambo hawakutaka kuwaficha wezi. Na hata nilipokuwa nikitoka uongozini tulikuwa tumebakisha watu 9 pekee kati ya watu zaidi ya 100 ambao walikuwa wakihusika na wizi wa mifugo. Kwa hivyo naomba serikali ikabili wezi bali si kujumuisha jamii nzima kwamba inaendeleza wizi wa mifugo.” Alisema.