SERIKALI YA UASIN GUSHU KUKUSANYA SHILINGI BILIONI 1.5 KABLA YA MWAKA WA KIFEDHA KUTAMATIKA

Serikali ya kaunti ya Uasin Gishu imesema kuwa inalenga kukusanya takriban shilingi bilioni 1.5 mapato yanayotokana na ulipaji ushuru kabla ya kutamatika kipindi cha kifedha cha mwaka 2021 – 2022.

Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret mkurugenzi wa idara ya ukusanyaji  ushuru kaunti hiyo CPA Jonah Lamai amesema kuwa kufikia sasa idara hiyo imekusanya shilingi milioni 890.

Lamai ameongeza kuwa wanatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 700 kutokana na malipo ya ada za shamba kabla ya tarehe 30 mwezi ujao.

Aidha Lamai ametoa wito kwa wafanya biashara na pia wamiliki wa ardhi ambao wana madeni ya awali kuhakikisha kwamba wanalipa kwa wakati ili kuiwezesha serikali ya kaunti hiyo kukusanya fedha zitakazofanikisha utoaji wa hudma bora kwa wakazi.